Published On: Fri, Jan 20th, 2017

MCHANGO WA KODI NA USHURU KATIKA KUTIMIZA AZMA YA KUWATUMIKIA WATANZANIA

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Katika uchaguzi mkuu wa Marekani wa mwaka jana, suala la kodi liibuka kwa kiasi kikubwa na hata kuathiri kampeni za urais wa chama cha Republican. Umuhimu wa kodi kwa taifa lolote duniani ikiwa ni pamoja na Marekani ulijidhihirisha wazi pale ambapo kashfa ya ukwepaji wa kulipa kodi ulioshukiwa kufanywa na mgombea wa chama cha Republican, Donald Trumph ulikaribia kumpatia mpizani wake Hilary Clinton ushindi.
Suala la kodi sio tu lilimuathiri Donald Trump katika kampeni zake, bali lilionesha umuhimu wa kodi kwa maendeleo ya taifa lolote duniani na hasa katika kutimiza wajibu wa msingi wa Serikali katika kuwatumikia wananchi wake kwa kutoa huduma zinazozingatia sifa, viwango na ubora ilivyojiwekea.
Ili kutekeleza wajibu huo, Serikali huandaa bajeti yake inayoanisha mipango na mikakati mbalimbali ya kukusanya fedha kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato ilivyojiwekea.
Katika kufikia malengo ya bajeti ya mwaka 2016/17 Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungani wa Tanzania imeongeza vyanzo vya mapato tofauti na vile vilivyozoeleka kama soda, sigara, bia, pombe kali, kodi za mishahara na tozo mbalimbali.
Baadhi ya maeneo ambayo kwa sasa serikali ya awamu ya tano tayari imeyaongenza kama vyanzo vipya vya mapato ni pamoja na kuongeza kodi mbalimbali kwenye simu (vocha na miamala), kodi ya majengo, kodi ya bidhaa za nje ikiwemo magari pamoja na kufuta misamaha ya kodi mbalimbali.
Akizungumza katika uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa barabara za juu Jijini Dar es Salaam April 16 mwaka jana, Rais Dkt. John Magufuli alisema Serikali imekusudia kupandisha bajeti ya fedha za maendeleo kutoka asilimia 26 mwaka 2015/16 hadi kufikia asilimia 40 mwaka 2016/17.
“Serikali ya Awamu ya Tano itaongeza nguvu katika upanuzi wa wigo wa kodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato”, Kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli wakati wa akifungua rasmi Bunge la 11 la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.
Rais alisisitiza ya kuwa Serikali yake itahakikisha kila mtu anayestahili kulipa kodi analipa kodi stahiki na kwa wakati ili kuharakisha maendeleo ya nchi ambayo yako nyuma ukiringanisha na nchi nyingine za ukanda wa Afrika mashariki. 
“Hatutasita kumchukulia hatua mtu yoyote atakaye kwepa kulipa kodi, tunawaomba wananchi mhakikishe mnapewa risiti kila mnaponunua bidhaa au huduma. Kodi ni kitu muhimu lazima kila mtu anayestahili kulipa kodi alipe” alifafanua Rais Magufuli.
Msisitizo mkuwa wa kukusanya kodi ambao Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania  amekuwa  akiuhubiri karibu katika ziara zake zote nchini, unaleta maswali mengi katika vichwa vya watanzania. Lakini swali muhimu zaidi ambalo kila mtanzania anapaswa kujiuliza ni hili; kwanini Mheshimiwa Rais Magufuli amelipatia suala la kodi kipaumbele cha kwanza kabisa katika vipaumbele vya serikali yake ya awamu ya tano?
Kupata majibu mazuri ya swali hili ni lazima kurudi nyuma miezi kama minne au mitano ambayo inatufikisha wakati wa kipinda cha mbio za kuelekea Ikulu ya magogoni. Katika sehemu zote ambazo mheshimiwa Magufuli alifanya kampeni zake hakusahau kuonesha dhamira yake ya kuwatumikia watanzania, “sintawaangusha,… nitawafanyia kazi kweli kweli”.
Kazi zote ambazo Mheshimiwa rais aliziahidi kuwafanyia watanzania, zinahitaji pesa kwa kiwango kikubwa sana. Hii ndio sababu kubwa inayomsukuma kupambana na mtu yeyote yule anayetumia vibaya pesa za serikali, ikiwa na pamoja na kuzuia kila mrija unaotoa pesa kwenye hazina ya serikali kwenda mahala pasipojulikana. Katika hili kila mtanzania ameshuhudia ziara za viongozi wa serikali kwenda nje ya nchi zikifutwa.
Zaidi ya kuzuia matumizi mabaya ya pesa za umma, rais Magufuli alitambua mapema kabisa ya kuwa pesa nyingi zitakazomuwezesha kuwatumikia wananchi, atazipata kwa kusimamia mapato yatokanayo na kodi mbali mbali. Katika hili pia watanzania wameshuhudia ziara nyingi sana za kushitukiza kwenye lango kuu la biashara na mapato ya nchi, bandari ya Dar es salaam. Lakini pia mabadiriko makubwa ya uongozi wa bandari na mamlaka ya mapato Tanzania (TRA).
Aidha, Mheshimiwa Magufuli alipokuwa akifungua rasmi Bunge la 11 la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, alionesha ni kwa kiasi gani alikuwa anahitaji pesa kwa maendeleo ya nchi aliposema ya kuwa Serikali yake itahakikisha kila senti inayoongezeka katika mapato ya Serikali inaelekezwa katika kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi na kuziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali ambayo inaipunguzia Serikali uwezo wake wa kuwahudumia wananchi. 
Taarifa kutoka Malaka ya Mapato Tanzania (TRA)  zinaonesha kuwa malengo ya mamlaka kwa sasa ni kuongeza Mapato ya ndani kwa kuimarisha ulipaji kodi wa hiari sambamba na kurahisisha ulipaji wa kodi hizo na kufanya maisha kuwa bora kwa wananchi.
Taarifa hiyo imejikita katika kutoa ufafanuzi kwa wananchi kodi na ushuru mbalimbali zinazotozwa na Malamka hiyo kwa lengo la kuimarisha mapato ya nchi ili kuwezesha kutatua baadhi ya changamoto na huduma bora kwa wananchi.
Aidha, inasema kuwa kila mwananchi anapaswa kujua kodi na ushuru mbalimbali zinazotozwa na Mamlaka hiyo ikiwemo kodi zinatozozwa kwa makampuni ambapo kodi kwenye mapato yote ya kampuni kiwango chake ni  asilimia 30 kwa wakazi na asilimia 30 kwa wasio wakazi.
Kwa upande wa Kodi ya mapato kwa makampuni yanapata hasara kwa miaka mitatu mfululizo viwango vyake ni asilimia 0.3 ya mauzo ya mwaka kwa wakazi na asilimia 0 kwa wasio wakazi.
Vile vile kodi ya mapato ya mtu binafsi kwa upande wa Tanzania Bara, mapato kwa mwezi kwa watu wenye mapato yasiozidi shilingi 170,000 hakuna kiwango chochote cha kodi kinachotozwa kwa mtu huyo, ambapo mapato yanayozidi shilingi 170,000 lakini hayazidi  360,000 atatakiwa kulipa kiwango cha kodi kwa asilimia 9.
Sambamba na hilo, viwango vya kodi ya mapato kwa watu binafsi wakazi wa Zanzibar , mapato yasiyozidi shilingi 105,000 kwa mwezi hakuna kiwango chochote cha kodi kinachotozwa, ambapo kwa yanayozidi shilingi 150,000 lakini hayazidi 360,000 kiwango cha kodi ni asilimia 13 kwa mwezi.
Taarifa hiyo inafafanua kuwa mapato ya mwezi ni pamoja na mshahara, malipo kwa kazi za ziada, bonsai, kamisheni na marupurupu mengine yatokanayo na ajira.
Kwa upande wa kodi za kuendeleza ufundi stadi (SDL), taarifa hiyo inasema kuwa kwa Tanzania Bara kiwango chake ni asilimia 4.5 ya malipo yote aliyolipa mwajiri kwa wafanyakazi wake kwa mwezi husika na asilimia 5 kwa Zanzibar.
Taarifa hiyo inasema zimo baadhi ya taasisi zinazosamehewa SDL ikiwemo Idara au Taasisi za Serikali ambazo zinaendeshwa kwa ruzuku ya Serikali, ofisi za kidiplomasia, Ummoja wa Mataifa na taasisi zake, taasisi za dini ambazo waajiriwa wake wameajiriwa kwa ajili ya kuendesha sehemu ya kuabudu, kutoa mafunzo ya dini na kuelimisha dini kwa ujumla.
Zingine ni mashirika yanayotoa misaada ya hiari yasiyojihusisha na biashara kwa namna yoyote ile, Serikali za mitaa pamoja na mwajiri wa shamba ambaye waajiriwa wanajihusisha moja kwa moja na shughuli za kilimo pekee.

Leave a comment

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>

Connect with us on social networks
Recommend on Google